Ulinganishi wa Fonolojia ya Kiswahili cha Bujumbura na Kiswahili cha Kivu

Authors

Abstract

Makala hii inalinganisha Kiswahili cha Bujumbura na Kiswahili cha Kivu ikibainisha upekee wa kifonolojia wa Kiswahili cha Bujumbura. Data zilitoka kwa wasailiwa 30, vipindi vya redio na maandiko mbalimbali. Usaili, usikilizaji makini na mapitio ya nyaraka ni mbinu zilizotumika kukusanyia data. Matokeo yameonesha ufanano na tofauti ndogo baina ya Kiswahili cha Bujumbura na cha Kivu. Kiswahili cha Bujumbura kina silabi huru na huzuia uwapo wa silabi yenye muundo wa I katikati au mwishoni mwa neno, sawa na Kiswahili cha Kivu. Mabadiliko ya kifonolojia kama vile udondoshaji wa irabu, usigano na uyeyushaji yamefanana kwa kiasi kikubwa katika Kiswahili cha Bujumbura na cha Kivu. Hata hivyo, Kiswahili cha Bujumbura kimetofautiana na Kiswahili cha Kivu kwa mpishano huru unaojitokeza baina ya irabu za nusu juu /e/ na /o/ na irabu za nusu chini /ɛ/, /ɔ/. Pia, fonimu /b/ hudhihirisha mpishano wa alofoni /b/ na /β/. Vilevile, Kiswahili cha Bujumbura hudhihirisha usigano ambapo konsonanti sighuna /k/ ya kiambishi cha kitenzi {ku-} hubadilika na kuwa konsonanti ghuna /g/. Ingawa matokeo ya makala hii yamedhihirisha ufanano wa kifonolojia katika Kiswahili cha Bujumbura na cha Kivu, tafiti kuhusu nyanja zingine za kiisimu zinahitajika ili kutambua ikiwa ni lahaja moja au la.

http://doi.org/10.56279/jk.v89i1.3

 

☍ View Article Analytics

Published

2026-06-30

Issue

Section

Articles