Nafasi ya Rasilimali Jadi katika Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira

Authors

  • Doroth Mosha Chuo Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam

Abstract

Rasilimali jadi ni miongoni mwa fani za fasihi simulizi kama vile semi, miviga, hadithi, maigizo na ushairi simulizi ambazo zimekuwapo tangu kale katika mfumo wa maisha ya mwanadamu. Rasilimali hizi zina utajiri wa kanuni na taratibu mbalimbali zinazoielekeza jamii husika kuhusu nyanja mbalimbali za kiuchumi, kiutamaduni, kisiasa, kijamii na kimazingira. Makala hii imechunguza nafasi ya rasilimali jadi katika kuhifadhi na kutunza mazingira, ambayo kwa kiasi kikubwa yameathiriwa na mabadiliko ya wakati, uvumbuzi, maendeleo ya sayansi na teknolojia na utandawazi. Maendeleo haya yamesababisha rasilimali jadi kutothaminiwa na kutambulika kama ilivyokuwa hapo awali, jambo lililochochea kufanyika kwa utafiti huu. Data za makala hii zilikusanywa katika mkoa wa Lindi, wilaya ya Kilwa, kata za Masoko, Somanga na Songosongo. Mbinu za ukusanyaji wa data zilihusisha mahojiano ya mtu mmoja mmoja na vikundi, ambao kutokana na tajiriba ya kazi zao, wameshuhudia mabadiliko ya mazingira katika maeneo ya baharini na nchi kavu. Vilevile, mbinu ya ushuhudiaji ilitumika ambapo mtafiti alishuhudia mandhari na utendaji wa matambiko ambayo yana ukuruba na mazingira ya jamii husika. Makala imeongozwa na Nadharia ya Uhakiki-Ikolojia ambayo inachunguza uhusiano baina ya fasihi na mazingira. Matokeo ya makala hii yanabainisha kuwa licha ya rasilimali jadi kuwa na hazina ya elimu jadi ya kuhifadhi mazingira, hazitambuliki na kuzingatiwa vya kutosha na jamii pana kama njia mojawapo ya kuhifadhi na kulinda mazingira. Maendeleo ya teknolojia na mabadiliko ya kijamii ni miongoni mwa vichocheo vinavyosababisha rasilimali jadi hizi kuendelea kufifia na pengine kupotea endapo hakutakuwa na mikakati ya kuziendeleza.

http://doi.org/10.56279/jk.v88i2.3

☍ View Article Analytics

Published

2026-01-29

Issue

Section

Articles