Sitiari ya Bahari katika Ushairi wa Kiswahili: Mifano kutoka Nyimbo Teule za Muziki wa Dansi
Abstract
Miongoni mwa mbinu za kisanaa zinazotumiwa na wasanii wa fasihi ni sitiari ambazo kwa hakika hutumiwa hata katika mawasiliano ya kawaida. Sababu ya kutumia sitiari ni kufafanua dhana dhahania au changamani kwa kutumia dhana zilizozoeleka ili kurahisisha uelewekaji wake. Miongoni mwa sitiari inayotumiwa katika mawasiliano ya kawaida na katika fasihi ya Kiswahili ni ile ya bahari. Kutokana na ukubwa na umuhimu wake katika maisha ya kila siku, hususani kwa watu wa upwa wa Afrika Mashariki, bahari inatazamwa kama gimba lenye masuala mengi, mazuri na mabaya. Lengo la makala hii ni kufafanua sitiari ya bahari inavyotumiwa katika ushairi wa Kiswahili, hususani nyimbo za muziki wa dansi za Kiswahili. Uchambuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Sitiari ya Kidhana ambayo inaeleza kuwa sitiari haiishii tu katika maneno bali huakisi fikra za jamii inayotumia sitiari hizo. Kwa kuwa fikra na tajiriba za watumiaji wa sitiari hufumbatwa katika kikoa chanzi, basi uchambuzi wetu umemakinikia zaidi sehemu ya kikoa chanzi cha sitiari ili kubaini fikra na tajiriba za bahari kama zinavyotumiwa katika nyimbo teule. Katika makala hii, sitiari za bahari zinaonesha kuwa, pamoja na umuhimu wake katika maisha, bahari ni sehemu hatari ambapo watumiaji wa bahari, hususani wavuvi na wasafiri, hupaswa kuwa waangalifu na wenye uzoefu wa hali ya juu ili kukabiliana na hatari zinazoweza kujitokeza. Vilevile, imeonekana kuwa bahari ni sehemu muhimu kwa sababu watu hupata chakula na huitumia kwa usafiri wa gharama nafuu.
DOI: http://doi.org/10.56279/jk.v88i2.6
