Simulizi ya Chemichemi Bikuri na Nafasi yake katika Utunzaji wa Mazingira

Authors

  • Geniva Kazinja University of Dar es Salaam

Abstract

Masuala ya utunzaji wa mazingira yameendelea kuzua mjadala mpana miongoni mwa wanamazingira na wanafasihi kutokana na ongezeko la uharibifu wa mazingira. Katika muktadha huo, fasihi hasa fasihi simulizi imejitokeza kama nyenzo muhimu ya kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu wajibu wa kimaadili wa kulinda mazingira. Makala hii inachunguza uhusiano uliopo kati ya masimulizi ya kimapokeo na utunzaji wa mazingira, kwa lengo la kuonesha namna simulizi hizo zinavyofanya kazi kama nyenzo za kielimu na kiutamaduni katika jamii za Kiafrika. Kupitia simulizi ya Chemichemi Bikuri kutoka Misenyi, mkoani Kagera, makala hii inafafanua jinsi jamii za Kiafrika zilivyounda mifumo ya kimaadili na kisheria kwa kutegemea imani za kiasili, masharti ya kijamii na vitisho vya kimitholojia ili kudhibiti uharibifu wa mazingira. Utafiti huu umeongozwa na Nadharia ya Uhakiki Ikolojia iliyoasisiwa na Glotfelty (1996), ambayo inalenga kuchunguza uhusiano kati ya binadamu na mazingira yake. Kupitia mtazamo wa uhakiki ikolojia, makala hii inadhihirisha kuwa uhifadhi wa mazingira ulihusishwa moja kwa moja na uhai na ustawi wa jamii, kwani mazingira safi yalichukuliwa kuwa msingi wa uhusiano bora wa binadamu na ulimwengu. Hivyo, makala hii inapendekeza kuzingatiwa kwa masimulizi ya kimapokeo kama rasilimali muhimu katika mijadala ya sasa kuhusu uhifadhi endelevu wa mazingira.

DOI: http://doi.org/10.56279/jk.v88i2.7

☍ View Article Analytics

Published

2026-03-08

Issue

Section

Articles