
Ujitokezaji wa Uduara wa Kiantonimu katika Vitomeo vya Kamusi Kuu ya Kiswahili Toleo la Tatu (BAKITA, 2022)
Citations by year
No citation data available yet.
Abstract
Baadhi ya vidahizo katika kamusi wahidiya huelezana kimaana kutegemea maneno yaliyounda ufafanuzi wa vidahizo hivyo. Sehemu ya ufafanuzi huo huunda uduara wa kileksikografia ambao maana zake huwa za kawaida au za unyume. Muunganiko wa kidahizo na taarifa zake zinazoujaza ufafanuzi huunda vitomeo. Makala hii imechunguza uduara wa kiantonimu uliojitokeza katika vitomeo vya Kamusi Kuu ya Kiswahili, Toleo la Tatu iliyotungwa na Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) mwaka 2022. Makala imechochewa na haja ya kuweka bayana uhusiano wa kiantonimu kati ya vidahizo na vifafanuzi vyake. Data zimekusanywa maktabani kwa njia ya usomaji wa matini. Vidahizo vyote 22,675 vya KKK3 kuanzia herufi A hadi Z vimeangaziwa kwa kuzipambanua antonimu zilizotumika kuimarisha maana zake. Kati ya vidahizo 22,675 vimepatikana 379 vilivyofafanuliwa kiantonimu. Vidahizo hivi vilichunguzwa zaidi ili kuzipata antonimu zilizoingizwa kama vidahizo kamili badala ya kutumika tu kwenye ufafanuzi. Nadharia Jumuishi ya Leksikografia imetumika kuchanganua data. Matokeo yameonesha kuwa, vidahizo 54 vya kiantonimu vimeunda jozi 27 zilizofafanuana. Antonimu zilizotumika kuvifafanua vidahizo, nazo zimeingizwa kama vidahizo vingine vilivyounda vitomeo vipya vyenye unyume. Uduara wa kiantonimu umejitokeza kwa misingi ya ujazo wa taarifa na mpangilio wa kialfabeti wa vidahizo. Katika ujazo wa taarifa kuna uduara-nusu na uduara-kamili. Kialfabeti, kuna uduara unaohusu mwongozano imara, mwongozano hafifu na mwachano wa vitomeo. http://doi.org/10.56279/jk.v89i1.5