Manyezi ya Utumwa katika Makutano ya Utumwa na Ukoloni na Athari yake katika Usemi wa Kitamaduni na Mtazamo wa Jamii za Afrika Mashariki

Authors

  • Ali H. Chembea Chuo Kikuu cha Pwani

Abstract

Utumwa ni suala linalozua si tu manyezi katika fasihi ya Kiswahili bali pia linaakisi utata wa kihistoria na kijamii katika Ukanda wa Afrika Mashariki. Fasihi ya Kiswahili imekuwa chemchemi yenye nguvu kueleza sauti za waliotengwa, kutambua hali halisi ya maisha ya utumwa, upinzani na ustahimilivu. Uchunguzi huu umeshughulikia makutano ya ukoloni na utumwa, ukionesha jinsi nguvu hizi zinavyoingiliana kuathiri usemi wa kitamaduni na mitazamo ya jamii. Kupitia diwani ya Sauti ya Dhiki iliyoandikwa na Abdilatif Abdalla na riwaya ya Kasri ya Mwinyi Fuad iliyoandikwa na Adam Shafi ndani ya mifumo mipana ya kihistoria, waandishi wameonesha mateso ya kihisiamoyo na ya kimwili ya watumwa, hasa katika kuangazia mapambano yao ya kupata uhuru na utu. Makala hii inachanganua umuhimu wa kuelewa utumwa si tu kama ukweli wa kihistoria bali kama masimulizi yenye nguvu ambayo yanaendelea kuvuma katika matini za fasihi ya Kiswahili. Hatimaye, uchunguzi huu umesawiri ufahamu wa kina wa athari za utumwa, ukiangazia jukumu lake katika kujenga utambulisho wa kitamaduni na kukuza diskozi za kijamii katika mapambano yanayoendelea ya haki na utu.

DOI: https://dx.doi.org/10.4314/kcl.v23i2.4

☍ View Article Analytics

Downloads

Published

2026-03-20