Ruwaza za Sinonimu zenye Asili ya Kiarabu katika Kiswahili

0 Article Views All time
0 Downloads All time
0 Citations Source: OpenAlex

Citations by year

No citation data available yet.

Abstract

Lugha ya Kiswahili ina muwasala wa muda mrefu na lugha mbalimbali za kigeni kama Kiarabu. Kuwapo kwa muwasala huo kumesababisha lugha ya Kiswahili kukopa maneno mengi kutoka lugha hiyo (Mbaabu, 2007; Gibbe, 2010). Maneno katika lugha hukopwa kutokana na sababu mbalimbali. Baadhi ya sababu hizo ni kukosekana kwa msamiati unaosimamia dhana ngeni ambazo hazifahamiki katika lugha pokezi na kasumba ya wazungumzaji kukopa maneno kutoka lugha za kigeni hata kama msamiati unaokopwa ulikwisha kukopwa kutoka lugha hiyo ya kigeni (Kiango, 1999). Matokeo ya ukopaji huo husababisha lugha kuwa na maneno mawili au zaidi yanayohusiana kimaana kutoka lugha ngeni moja. Hali hii husababisha kuibuka kwa sinonimu. Lugha inapokuwa na sinonimu mbalimbali husababisha kuibuka kwa ruwaza za sinonimu. Makala hii inachunguza ruwaza za sinonimu zenye asili ya Kiarabu katika Kiswahili kwa kutumia mifano kutoka Kamusi ya Kiswahili Sanifu, Toleo la 4 (KKS4) (2019). Ili kufikia azma ya kuchunguza ruwaza hizo, data za makala hii zimekusanywa kutoka kwenye kamusi tajwa. Ukusanyaji wa data umefanyika kwa kutumia mbinu ya uchambuzi wa matini. Data zilizokusanywa zimechambuliwa kwa kutumia mbinu ya maudhui na kuongozwa na Nadharia ya Vijenzi Semantiki. Kwa ujumla, makala hii imebaini kuwa lugha ya Kiswahili ina ruwaza sita za sinonimu za mkopo kutoka Kiarabu. Ruwaza hizo ni ruwaza ya uwili, ya utatu, ya unne, ya utano, ya usita na ya usaba. Makala hii inapendekeza kufanyika kwa tafiti zaidi kuhusu maneno ya mkopo yanavyoibua sinonimu kutoka lugha nyingine kama Kiingereza, Kihindi au Kiajemi ili kubaini ruwaza zake DOI: https://dx.doi.org/10.4314/kcl.v24i1.2