
Motifu ya Utumwa na Utabaka ndani ya Kisiwa cha Pate: Utendi wa Mwanakupona kama Tarihi ya Kihistoria
Citations by year
No citation data available yet.
Abstract
Utendi wa Mwanakupona ni utenzi uliotungwa na mwanamke, Mwanakupona binti Mshamu Nabhany, kumnasihi bintiye Mwana Hashima bint Shee Mataka na kumshauri namna ya kuwa mke mwema kwa mumewe. Mwanakupona alikuwa binti wa Mshamu Nabhany na mkewe Mohammed Is-Haq Mbarak. Alizaliwa mjini Pate mwaka 1810 (Senkoro, 2011). Awali Utendi wa Mwanakupona ulitungwa kwa hati za Kiarabu. Katika fasihi ya Kiswahili, kazi ya kihistoria ya Uhuru wa Watumwa (1934) iliyotungwa na James Mbotela ndiyo maarufu na inaangazia motifu ya watumwa. Hata hivyo, kuna kazi nyingine za fasihi ya Kiswahili kuhusu utumwa. Wapo wahakiki wengine ambao wanauangalia Utendi wa Mwanakupona kama utumwa wa kimawazo au utumwa wa ukandamizaji wa wanawake. Makala imechunguza motifu ya utumwa na utabaka katika Kisiwa cha Pate kilichoko kaunti ya Lamu. Mazungumzo ya kikundi lengwa yalishirikisha baadhi ya wakazi wa kisiwa cha Pate na maeneo ya Lamu ambao waliulizwa mitazamo yao kuhusu mada husika na kutoa fursa ya kubadilishana mawazo na wengine ambao walikuwa na maoni tofauti. Tulisikiliza, kuandika madokezo, na pia kurekodi mazungumzo katika mazingira yao ili kupata taarifa za moja kwa moja kuhusu mada ya utafiti. Vilevile, uchanganuzi wa data ya pili ulifanyika katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Nairobi. Utafiti uliongozwa na Nadharia ya Ufeministi wa Kiafrika. DOI: https://dx.doi.org/10.4314/kcl.v23i2.6