
Kategoria za Utumwa katika Fasihi ya Kiswahili: Uchunguzi wa Kazi Teule
Citations by year
No citation data available yet.
Abstract
Utumwa ni mfumo ambao hulazimisha watu kufanya kazi au jambo fulani bila malipo au ridhaa. Kuna aina kuu mbili za utumwa, yaani utumwa wa kijadi na utumwa wa kisasa3. Utumwa wa kijadi unahusu watu kuuzwa kama bidhaa na kwenda kutumikishwa sehemu kama vile kwenye mashamba makubwa, migodini na majumbani. Ni utumwa ulioanza zamani sana na ulikuwapo katika jamii kwa karne nyingi. Madhara ya utumwa wa kijadi bado hayajafutika katika historia za jamii husika. Kwa upande mwingine, utumwa wa kisasa ni ule unaojitokeza kwa namna nyingi kama vile: utumwa wa kifikra, kimapenzi, madeni, na kutumikisha watoto wadogo. Aina hii ya utumwa, licha ya kuonekana kuwa umeshika kasi sana katika zama hizi za utandawazi, kwa hakika, baadhi ya aina zake zimekuwa katika jamii kwa muda mrefu. Makala hii imejadili namna fasihi ya Kiswahili inavyosawiri utumwa wa kijadi na aina anuwai za utumwa wa kisasa. Kwa kutumia Nadharia ya Mwingilianomatini, riwaya nne za fasihi ya Kiswahili - Uhuru wa Watumwa (1934), Kasri ya Mwinyi Fuad (1987), Kwaheri Iselamagazi (1992) na Miradi Bubu ya Wazalendo (1995) zimechunguzwa ili kuweka bayana suala hili. Imebainika kuwa utumwa wa kisasa una madhara ambayo hayajulikani mapema ikilinganishwa na utumwa wa kijadi kwa sababu madhara hayo hayaonekani waziwazi kwa kuwa yapo ndani ya utu wa mhusika. Pia, utumwa wa kisasa, kama vile utumwa wa kifikra na utumwa wa madeni unachangia katika utokeaji na/au uimarishaji wa utumwa wa kijadi. DOI: https://dx.doi.org/10.4314/kcl.v23i2.2