
Minyiri ya Utumwa-Lugha na Mtanziko wa Fikra za Kikoloni miongoni mwa Waafrika
Citations by year
No citation data available yet.
Abstract
Maana ya utumwa imekuwa sehemu mojawapo ya mada katika mijadala ya wanazuoni hasa baada ya mwaka 1926. Mpaka mwaka 2012, bado kulikuwa na mjadala wa kisheria kuhusu maana ya utumwa. Mijadala hii haikuangalia sana suala la lugha kama nyenzo yenye kuingiza dhana ya kipekee katika maana ya utumwa. Hata hivyo, ni wazi kuwa wakati wa utumwa wa Waarabu, lugha ilitumika kuufanikisha utumwa. Lugha iliubeba utumwa. Wakati wa ukoloni mkongwe, lugha za kikoloni zilijenga matabaka ya kitumwa. Minyiri ya utumwa-lugha ikajiviringa na kuwavunganiza watumwa kifikra na kuwafanya wajikane. Wakati huu wa ukoloni mamboleo, utumwa-lugha umeifanya fikra ya aliyetawaliwa kushikwa na minyiri ya kikoloni kiasi cha kujikuta katika mtanziko: alikotoka hakujui, na kama kuna aendako, hakufahamu. Makala hii ikiongozwa na mawazo ya Frantz Fanon kuhusu lugha (2008), imetumia dhana ya utumwa-lugha kujadili jinsi lugha za watawala wa kikoloni barani Afrika zinavyotokeza utumwa wa kifikra, ambao hatimaye unaharibu misingi mikuu ya kuwapo kwa Mwafrika. Kupitia utumwa-lugha, Waafrika wameachwa katika mtanziko mkubwa wenye mivutano ya ndani inayojibadilisha kuwa minyiri isiyoweza kukatwa na kungâolewa bila ya kuwa na mapinduzi ya kifikra. DOI: https://dx.doi.org/10.4314/kcl.v23i2.5