
Udhihirikaji wa Utumwa katika Manamba: Uchunguzi Kifani wa Riwaya ya Miradi Bubu ya Wazalendo
Citations by year
No citation data available yet.
Abstract
Watu kutoka Afrika, hususan watu weusi, ni mbari iliyoathirika vibaya kutokana na maendeleo ya madola mbalimbali barani Afrika na maendeleo ya ubeberu barani Ulaya. Utumwa na ukoloni ni miongoni mwa matukio yaliyowaathiri Waafrika kiuchumi, kijamii na kisiasa, na yalimwondolea mtu mweusi hadhi ya ubinadamu wake kwa kumfanya kama mnyama au bidhaa. Madhara ya biashara ya utumwa na ukoloni bado yapo bayana. Katika Ukanda wa Afrika Mashariki, biashara ya utumwa ilikomeshwa na Waingereza katika nusu ya pili ya karne ya 19. Inaelezwa kuwa Waingereza walitokomeza biashara ya utumwa kwa misingi ya kiutu. Dai hili, ambalo lilishamiri kutokana na ongezeko la propaganda za kibeberu katika karne ya 19, linadokeza huruma ya Waingereza kutokana na udhalilishaji kwa watumwa wa Kiafrika. Hata hivyo, baadhi ya matendo waliyotendewa Waafrika wakati wa ukoloni wa Waingereza haohao, hususan katika mfumo wa manamba[1] hayatofautiani sana na yale yaliyofanyika wakati wa utumwa. Kwa kutumia kiunzi cha kinadharia cha uingiaji, tajiriba na utokaji katika utumwa kama kilivyofafanuliwa na van der Linden (2016), makala hii inalenga kujadili sura za utumwa katika mfumo wa manamba kama zinavyosawiriwa katika riwaya ya Miradi Bubu ya Wazalendo (Ruhumbika, 1995). Kwa kutumia kiunzi teule, imebainika kuwa michakato ya kuingia, tajiriba za utokaji katika manamba na utumwani inafanana kwa kiasi fulani. Katika riwaya teule, matendo yaliyofanywa kwa manamba yanashabihiana na yale yaliyowasibu watumwa pahala pengine duniani, hususan Afrika Mashariki na Marekani. Makala imehitimishwa kuwa mifumo yote miwili, yaani utumwa na ule wa manamba haikuzingatia utu.