
Usawiri wa Wahusika wa Ajabuajabu katika Riwaya Teule za Kihalisiajabu za Shaaban Robert na za Euphrase Kezilahabi
Citations by year
No citation data available yet.
Abstract
Wahakiki na wataalamu mbalimbali wa kazi za fasihi wamejadili kwa mapana usawiri wa wahusika wa ajabuajabu. Miongoni mwao, kuna wanaobainisha jinsi wanavyojitokeza katika kazi za fasihi, namna wanavyoweza kuakisi uhalisia wa maisha katika jamii na kile kilichokusudiwa na mtunzi katika kuwatumia. Pamoja na kazi hizo kuchangia katika kuelewa kazi za fasihi zinazotumia wahusika wa ajabuajabu, aina za wahusika wa ajabuajabu hazijajadiliwa kwa kuzingatia upekee na umuhimu wake. Makala hii inabainisha aina za wahusika wa ajabuajabu kama zinavyojitokeza katika riwaya za Kiswahili za kihalisiajabu kwa kuangazia riwaya za Kusadikika (1951) na Adili na Nduguze (1952) za Shaaban Robert na Nagona (1990) na Mzingile (1991) za Euphrase Kezilahabi. Riwaya hizo ziliteuliwa baada ya kusoma riwaya mbalimbali zenye wahusika wa ajabuajabu na kubaini kuwa ndizo zenye data toshelevu zinazosadifu mahitaji ya makala hii. Data zilikusanywa kutoka vitabu teule kwa kutumia mbinu ya usomaji matini. Uchambuzi na uwasilishaji wa data katika makala hii umeongozwa na Nadharia ya Uhalisiajabu ya Franz Roh (1925) kwa kutumia mkabala wa kitaamuli. Nadharia hii imewezesha pia kuwabainisha wahusika wa ajabuajabu katika riwaya teule. Kwa kuzingatia kigezo cha kimaana, imebainishwa kuwa Shaaban Robert na Euphrase Kezilahabi wametumia aina za wahusika wa ajabuajabu kusawiri hali na matukio halisi katika jamii zao. DOI: https://doi.org/10.56279/mulika.na44t2.7