Uchunguzi wa Maumbo ya Wingi wa Heshima kwenye Kategoria za Kileksika za Lugha ya Kimatengo
Abstract
Wingi wa heshima ni dhana ya kiisimujamii ambayo haijaelezwa vya kutosha kuhusu fasili na uwasilishwaji wake kwenye kategoria za kileksika katika lugha za Kibantu, ikijumuishwa lugha ya Kimatengo[1]. Aidha, kuna ukanganyifu wa kuchukulia wingi wa heshima kama dhana ya upole kwenye isimujamii za lugha za Kibantu. Lengo la makala hii ni kuchunguza uwasilishaji wa maumbo ya wingi wa heshima kwenye kategoria za kileksika yanayotumiwa kumrejelea mtu kwa heshima katika jamii ya Wamatengo kutegemeana na hadhi yake. Data za utafiti huu zilikusanywa kwa mbinu za usaili, majadiliano ya vikundi lengwa, na ushuhudiaji shiriki. Data hizo zilikusanywa kutoka kwa wazungumzaji wazawa wa Kimatengo waishio wilayani Mbinga, mkoani Ruvuma. Uchambuzi wa data umeongozwa na Nadharia ya Upole ya Brown na Levinson (1987). Nadharia hii inaeleza kwamba, katika mazungumzo yoyote, kuna uwezekano kwa mzungumzaji kuonekana amemdhihaki au kumkejeli msikilizaji kwa aina ya maneno yanayotumiwa. Matokeo ya uchunguzi huu yanaonesha kuwa, katika Kimatengo, mofu za wingi wa heshima huwasilishwa kwenye kategoria za kileksika za nomino ({a}), viwakilishi ({a}, {b}), vivumishi ({a}) na vitenzi ({a}, {n}, {m}).
