Uamilifu wa Mofu {(-)i-} katika Kiswahili Kinachozungumzwa nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Abstract
Makala hii inachunguza uamilifu wa mofu {(-)i-} katika Kiswahili kinachozungumzwa nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Data zilizotumiwa zilikusanywa kutoka katika vipindi mbalimbali vya lugha ya Kiswahili vya redio zinazosikika mjini Bujumbura nchini Burundi, na Uvira, Bukavu na Goma katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Redio husika ni Redio-Televisheni ya Taifa ya Burundi (Radio-Télévision Nationale du Burundi, RTNB), Redio-Televisheni Isanganiro (Radio Télévision Isanganiro), Redio Bonesha FM, Redio Maendeleo ya Bukavu Kusini na Redio ya Umma ya Kivu Kusini (Radio Communautaire Thématique). Mbinu ya usikilizaji makini katika kusikiliza redio na uandishi zilitumiwa katika kukusanya data ambazo zilichanganuliwa kwa njia ya uchambuzi wa maumbo ya maneno. Nadharia ya Mofolojia ya Muunganiko wa Mofu ya Fradin (2003) na Nadharia ya Umiliki na Ufungati ya Chomsky (1981) ndizo zilizoongoza utafiti huu. Uchunguzi wa data ulidhihirisha mambo kadhaa. Kwanza, mofu {(-)i-} ambayo kwa kawaida wingi wake ni {zi-} huweza kuwakilisha ngeli zingine zozote katika neno husika na kuwa kibadala chake. Pili, matumizi ya mofu {(-)i-} hayazingatii idadi, hali ambayo huifanya kuashiria ama umoja au wingi. Tatu, huwa na uamilifu wa kiambishi cha upatanisho wa kisarufi. Kutokana na matokeo ya utafiti huu, ingawa mofu {(-)i-} ina uamilifu wa kimofosintaksia, hudhihirisha kutopatana kwa vipashio vya tungo katika Kiswahili kinachozungumzwa nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
